5 Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 6 Wakawaoa binti zao, nao wakawatoa binti zao waolewe na wana wa hayo mataifa, na kuitumikia miungu yao.
15 Waisraeli wakamlilia tena Bwana, naye akawapa mwokozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera, Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi. 16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga wenye ukatao kuwili, urefu wake ni kama dhiraa moja,[c] akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake kwenye paja lake la mkono wa kuume. 17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, ambaye alikuwa mtu mnene sana. 18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru aliwaruhusu waende zao. 19 Yeye mwenyewe akafuatana nao hadi kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwa ajili yako.”
20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kwenye kiti chake, 21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake. 22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga. 23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu na kuifunga kwa funguo.
24 Baada ya kuondoka, watumishi wakaja na kukuta milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka amejipumzisha kwenye chumba cha ndani cha nyumba yake ya majira ya kiangazi.” 25 Wakangoja hata wakawa na fadhaa, basi wakati hakufungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.
26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira. 27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.
28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Bwana amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakuacha mtu yeyote kuvuka. 29 Wakati huo wakawaua Wamoabu watu waume wapatao 10,000 ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa; hakuna mtu yeyote aliyetoroka. 30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.