6 Baada ya siku arobaini Noa akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina 7 na akamtoa kunguru, akawa akiruka kwenda na kurudi mpaka maji yalipokwisha kukauka juu ya nchi. 8 Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya uso wa ardhi. 9 Lakini hua hakupata mahali pa kutua kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Noa ndani ya safina. Noa akanyoosha mkono akamchukua yule hua akamrudisha ndani ya safina. 10 Noa akangojea siku saba zaidi kisha akamtoa tena hua kutoka safina. 11 Wakati hua aliporejea kwa Noa jioni, alikuwa amechukua katika mdomo wake jani bichi la mzeituni, lililochumwa wakati ule ule! Ndipo Noa akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya uso wa dunia. 12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Noa.
13 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 14 Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa.
15 Ndipo Mungu akamwambia Noa, 16 “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao. 17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
18 Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao. 19 Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine.