2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. 6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.
7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? 8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita. 9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10 Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
<- Wagalatia 4Wagalatia 6 ->