21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote. 22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.” 23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.
24 Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi, 25 nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Israeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu. 26 Niliwapimia talanta 650†Talanta 650 za fedha ni sawa na tani 25. za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia moja,‡Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75. talanta mia moja za dhahabu, 27 mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja,§Darkoni 1,000 ni sawa na kilo 8.5. na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu.
28 Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Bwana. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Bwana, Mungu wa baba zenu. 29 Vilindeni kwa uangalifu mpaka mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Bwana katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.” 30 Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.
31 Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu kwenye siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyangʼanyi. 32 Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu.
33 Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, pia walikuwako Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua na Noadia mwana wa Binui. 34 Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule.
35 Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba na mbuzi dume kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana. 36 Pia walikabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa Ngʼambo ya Mto Frati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.
<- Ezra 7Ezra 9 ->