1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli 3 uiambie: ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu. 4 Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utakuwa wazi dhidi ya kila mmoja kuanzia kusini mpaka kaskazini. 5 Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi Bwana nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’
6 “Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi. 7 Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatokea, asema Bwana Mwenyezi.”
8 Neno la Bwana likanijia, kusema: 9 “Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo:
“ ‘Upanga, upanga,
ulionolewa na kusuguliwa:
10 umenolewa kwa ajili ya mauaji,
umesuguliwa ili ungʼae
kama umeme wa radi!
“ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo.
11 “ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa,
ili upate kushikwa mkononi,
umenolewa na kusuguliwa,
umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.
12 Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu,
kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu;
u dhidi ya wakuu wote wa Israeli.
Wametolewa wauawe kwa upanga
pamoja na watu wangu.
Kwa hiyo pigapiga kifua chako.
13 “ ‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema Bwana Mwenyezi.’
14 “Hivyo basi, mwanadamu, tabiri
na ukapige makofi.
Upanga wako na upige mara mbili,
naam, hata mara tatu.
Ni upanga wa kuchinja,
upanga wa mauaji makuu,
ukiwashambulia kutoka kila upande.
15 Ili mioyo ipate kuyeyuka
na wanaouawa wawe wengi,
nimeweka upanga wa kuchinja
kwenye malango yao yote.
Lo! Umetengenezwa
umetemete kama umeme wa radi,
umeshikwa kwa ajili ya kuua.
16 Ee upanga, kata upande wa kuume,
kisha upande wa kushoto,
mahali popote makali yako
yatakapoelekezwa.
17 Mimi nami nitapiga makofi,
nayo ghadhabu yangu itapungua.
Mimi Bwana nimesema.”
18 Neno la Bwana likanijia kusema: 19 “Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini. 20 Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome. 21 Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama. 22 Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka vyombo vya kuvunjia boma, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka vyombo vya kuvunjia boma kwenye malango, kuweka jeshi kuzunguka na kufanya uzingiraji. 23 Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha juu ya uovu wao na kuwachukua mateka.
24 “Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu enyi watu mmekumbusha uovu wenu kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mfanyayo, kwa kuwa mmefanya jambo hili, mtachukuliwa mateka.
25 “ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yako imewadia, ambaye wakati wako wa adhabu umefikia kilele chake, 26 hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa na aliyekwezwa atashushwa. 27 Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya mpaka aje yule ambaye ndiye mwenye haki nao; yeye ndiye nitakayempa.’
28 “Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kuhusu Waamoni na matukano yao.