1 Kisha tukageuka tukakwea kufuata njia iliyoelekea Bashani, Ogu mfalme wa Bashani akaondoka na jeshi lake lote kupigana na sisi huko Edrei. 2 Bwana akaniambia, “Usimwogope kwa kuwa nimekwisha mkabidhi mikononi mwako pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Umfanyie sawasawa na ulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
3 Hivyo Bwana Mungu wetu pia akamweka Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote mikononi mwetu. Tuliwaangamiza wote, hakubakia hata mmoja. 4 Wakati huo tuliteka miji yake yote. Hakuna mji hata mmoja kati ya ile sitini ambao hatukuuteka, yaani eneo lote la Argobu, utawala wa Mfalme Ogu katika Bashani. 5 Miji yote hii ilijengewa ngome zenye kuta ndefu zenye malango na makomeo, pia kulikuwako na vijiji vingi ambavyo havikujengewa kuta. 6 Tuliwaangamiza kabisa, kama tulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Heshboni, tukiangamiza kila mji, yaani wanaume, wanawake na watoto. 7 Lakini wanyama wote wa kufuga pamoja na nyara kutoka kwenye miji yao tulichukua vikawa vyetu.
8 Hivyo kwa wakati huo tukachukua kutoka kwa wafalme hawa wawili wa Waamori nchi ya mashariki ya Yordani, kutoka Bonde la Arnoni mpaka kufika kwenye Mlima Hermoni. 9 (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri.) 10 Tuliteka miji yote kwenye uwanda wa juu, Gileadi yote, Bashani yote mpaka kufika Saleka na Edrei, miji ya utawala wa Ogu huko Bashani. 11 (Mfalme Ogu wa Bashani ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa mabaki ya Warefai. Kitanda chake kilikuwa cha chuma chenye urefu wa dhiraa tisa*Dhiraa tisa ni sawa na mita 4. na upana wa dhiraa nne.†Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8. Mpaka sasa kinaweza kuonekana katika mji wa Waamoni wa Raba.)
12 Katika nchi tuliyoiteka wakati ule, niliwapa kabila la Reubeni na Gadi eneo lililoko kaskazini la Aroeri kando ya Bonde la Arnoni, na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake. 13 Kisha nusu ya kabila la Manase niliwapa sehemu ya Gileadi iliyobaki pamoja na Bashani yote, ambayo ilikuwa utawala wa Ogu. (Eneo lote la Argobu katika Bashani lilikuwa linajulikana kama nchi ya Warefai. 14 Yairi, mzao wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu hadi kufikia mpaka wa Wageshuri na Wamaaka, ukaitwa kwa jina lake; kwa hiyo mpaka leo hii Bashani inaitwa Hawoth-Yairi.) 15 Nikampa Makiri nchi ya Gileadi. 16 Lakini niliwapa Wareubeni na Wagadi eneo kuanzia Gileadi hadi Bonde la Arnoni (katikati ya bonde ulikuwa ndio mpaka), kuelekea mpaka Mto Yaboki, ambao ndio mpaka wa Waamoni. 17 Kwa upande wa magharibi mpaka wao ulikuwa Yordani katika Araba, toka ziwa Galilaya hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), kwenye miteremko ya Pisga upande wa mashariki.
18 Wakati huo nilikuamuru: “Bwana Mungu wako amekupa nchi hii uimiliki. Lakini ni lazima wanaume wenu wote wenye uwezo, wakiwa wamejiandaa tayari kwa vita, wavuke ngʼambo wakiwatangulia ndugu zako Waisraeli. 19 Lakini wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu (kwani najua mnayo mifugo mingi) wanaweza kukaa katika miji niliyowapa, 20 mpaka hapo Bwana atakapowapa ndugu zenu kupumzika kama alivyowapa ninyi, wao pia wamiliki ile nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, ngʼambo ya Yordani. Baada ya hapo, kila mmoja wenu anaweza kurudi kwenye milki niliyowapa.”
23 Wakati huo nilimsihi Bwana: 24 “Ee Bwana Mwenyezi, umemwonyesha mtumishi wako ukuu wako na mkono wako wenye uweza. Kwa kuwa ni mungu yupi aliye mbinguni au duniani anayeweza kufanya kazi na matendo makuu kama ufanyayo wewe? 25 Acha niende nikaione hiyo nchi nzuri ngʼambo ya Yordani, ile nchi nzuri ya vilima na Lebanoni.”
26 Lakini kwa sababu yenu Bwana alinikasirikia na hakutaka kunisikiliza. Bwana aliniambia, “Hilo latosha; usiseme nami jambo hili tena. 27 Kwea juu ya kilele cha Pisga uangalie magharibi, kaskazini, kusini na mashariki. Iangalie hiyo nchi kwa macho yako, kwa vile wewe hutavuka Yordani. 28 Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na umtie nguvu, kwa kuwa yeye atawaongoza watu hawa hadi ngʼambo na kuwarithisha nchi utakayoiona.” 29 Kwa hiyo tulikaa kwenye bonde karibu na Beth-Peori.
<- Kumbukumbu La Torati 2Kumbukumbu La Torati 4 ->-
Dhiraa tisa ni sawa na mita 4.
- b Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8.