Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
16
Pasaka
(Kutoka 12:1-20)

1 Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Bwana Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku. 2 Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Bwana Mungu wenu kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo au la ngʼombe, mahali pale ambapo Bwana atapachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. 3 Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili kwamba siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri. 4 Chachu isionekane katika mali zenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe mpaka asubuhi.

5 Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Bwana Mungu wenu amewapa, 6 isipokuwa mahali atakapopachagua kama makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo ndipo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni, jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri. 7 Okeni na mle mahali pale ambapo Bwana Mungu wenu atakapopachagua, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu. 8 Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Bwana Mungu wenu na msifanye kazi.

Sikukuu Ya Mavuno
(Kutoka 34:22; Walawi 23:15-21)

9 Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka. 10 Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Bwana Mungu wenu kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Bwana Mungu wenu amewapa. 11 Shangilieni mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua kama makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane waishio miongoni mwenu. 12 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.

Sikukuu Ya Vibanda
(Walawi 23:33-43)

13 Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao yenu ya nafaka na kukamua zabibu. 14 Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu. 15 Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Bwana Mungu wenu katika mahali atakapopachagua Bwana. Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.

16 Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Bwana mikono mitupu: 17 Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki.

Waamuzi
18 Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Bwana Mungu wenu anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa. 19 Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. 20 Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa.
Kuabudu Miungu Mingine
21 Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Bwana Mungu wenu, 22 wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Bwana Mungu wenu anavichukia vitu hivi.

<- Kumbukumbu La Torati 15Kumbukumbu La Torati 17 ->
  • Kumbukumbu La Torati