4 (Yonathani mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa mlemavu miguu yote miwili. Alikuwa na miaka mitano wakati habari kuhusu Sauli na Yonathani zilipofika kutoka Yezreeli. Yaya wake akambeba ili kukimbia, lakini yaya alipokuwa anaharakisha kuondoka, mtoto alianguka akawa kiwete. Jina lake aliitwa Mefiboshethi.)
5 Basi Rekabu na Baana, wana wa Rimoni Mbeerothi wakaenda nyumbani kwa Ish-Boshethi, nao walifika huko wakati alipokuwa kwenye mapumziko yake ya mchana. 6 Wakaingia kwenye chumba cha ndani kana kwamba wanachukua ngano, wakamchoma Ish-Boshethi mkuki wa tumboni. Ndipo Rekabu na Baana nduguye wakatoroka.
7 Walikuwa wameingia ndani ya nyumba wakati alipokuwa amelala kitandani chumbani kwake. Baada ya kumchoma mkuki na kumuua, walikata kichwa chake. Wakiwa wamekichukua, walitembea usiku kucha kwa njia ya Araba. 8 Wakamletea Daudi kichwa cha Ish-Boshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, “Hiki hapa kichwa cha Ish-Boshethi mwana wa Sauli, adui yako, aliyejaribu kuondoa uhai wako. Siku hii ya leo Bwana amemlipia kisasi mfalme bwana wangu dhidi ya Sauli na mzao wake.”
9 Daudi akawajibu Rekabu na Baana nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka taabu zote, 10 yule mtu aliponiambia, ‘Sauli amekufa,’ akadhani ananiletea habari njema, nilimkamata, nikamuua huko Siklagi. Hiyo ndiyo zawadi niliyompa kwa ajili ya taarifa yake! 11 Je, ni mara ngapi zaidi wakati watu waovu wamemuua mtu asiye na hatia akiwa ndani ya nyumba yake mwenyewe na kwenye kitanda chake mwenyewe? Je, sasa nisidai damu yake mikononi mwenu na kuwaondoa duniani?”
12 Kwa hiyo Daudi akawaamuru watu wake, wakawaua. Wakakata mikono yao na miguu, na kutundika viwiliwili vyao kando ya dimbwi huko Hebroni. Lakini wakakichukua kichwa cha Ish-Boshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.
<- 2 Samweli 32 Samweli 5 ->