Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
15
1 Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa. 2 Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu. 3 Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Uwezo, matendo yako ni makuu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli! 4 Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yameonekana na wote.” 5 Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu. 6 Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo Hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa, na kanda za dhahabu vifuani mwao. 7 Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. 8 Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa makubwa saba ya wale malaika saba.

<- UFUNUO WA YOHANA 14UFUNUO WA YOHANA 16 ->