13
1 Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!” 2 Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.” 3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha, 4 “Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?” 5 Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu. 6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, Mimi ndiye! nao watawapotosha watu wengi. 7 Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado. 8 Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto. 9 “Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao. 10 Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote. 11 Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu. 12 Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 13 Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa. 14 “Mtakapoona Chukizo Haribifu limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani. 15 Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu. 16 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake. 17 Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo! 18 Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi. 19 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena. 20 Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo. 21 “Basi mtu akiwaambieni, Tazama, Kristo yupo hapa! au Yupo pale! msimsadiki. 22 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana. 23 Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea. 24 “Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza. 25 Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa. 26 Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu. 27 Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu. 28 “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 29 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana. 30 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia. 31 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 32 “Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. 33 Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini. 34 Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho. 35 Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi. 36 Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala. 37 Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!”
<- MARKO MTAKATIFU 12MARKO MTAKATIFU 14 ->