11
1 Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. 2 Yohane mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, 3 wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” 4 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: 5 vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. 6 Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami.” 7 Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? 8 Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. 9 Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. 10 “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Tazama, hapa namtuma mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako. 11 Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. 12 Tangu wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. 13 Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi. 14 Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Eliya ambaye angekuja. 15 Mwenye masikio na asikie! 16 “Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine: 17 Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia! 18 Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: Amepagawa na pepo. 19 Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: Mtazameni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wahalifu! Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.” 20 Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya: 21 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu. 22 Hata hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na Sidoni. 23 Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. 24 Lakini nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko kwako wewe.” 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo. 26 Naam Baba, ndivyo ilivyokupendeza. 27 “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha. 28 Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. 30 Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
<- MATHAYO MTAKATIFU 10MATHAYO MTAKATIFU 12 ->