1 Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni. 2 Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Ninyi mmejilundikia mali katika siku hizi za mwisho! 4 Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana, Mwenye Nguvu. 5 Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmemhukumu na kumwua mtu asiye na hatia, naye hakuwapigeni. 7 Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno mazuri. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. 8 Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia. 9 Ndugu zangu, msinung'unikiane ninyi kwa ninyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia. 10 Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana. 11 Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema. 12 Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni “Ndiyo” kama maana yenu ni ndiyo, na “La” kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu. 13 Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14 Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. 15 Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa. 16 Basi, ungamanianeni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi. 17 Eliya alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake. 19 Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha, 20 fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.
<- WARAKA WA YAKOBO 4