Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
WARAKA WA KWANZA WA PAULO MTUME KWA

TIMOTHEO

1 Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, 2 nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. 3 Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. 4 Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. 5 Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. 7 Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza. 8 Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo. 9 Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale; 10 sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli. 11 Mafundisho hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri. 12 Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, 13 ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. 14 Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. 15 Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, 16 lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele. 17 Kwake yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee—kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. 18 Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, 19 na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. 20 Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

1 TIMOTHEO 2 ->