1 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ni Kristo, huyo ni mtoto wa Mungu; na, anayempenda mzazi humpenda pia mtoto wa huyo mzazi. 2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu: Kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake; 3 maana kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na, amri zake si ngumu, 4 maana kila aliye mtoto wa Mungu anaweza kuushinda ulimwengu. Hivi ndivyo tunavyoushinda ulimwengu: kwa imani yetu. 5 Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. 6 Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake. Hakuja kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Naye Roho anashuhudia kwamba ni kweli, kwani Roho ni ukweli. 7 Basi, wako mashahidi watatu: 8 Roho, maji na damu; na ushahidi wa hawa watatu waafikiana. 9 Ikiwa twaukubali ushahidi wa binadamu, ushahidi wa Mungu una uzito zaidi; na huu ndio ushahidi alioutoa Mungu mwenyewe juu ya Mwanae. 10 Anayemwamini mwana wa Mungu anao ushahidi huo ndani yake; lakini asiyemwamini Mungu, anamfanya yeye kuwa mwongo, maana hakuamini ushahidi alioutoa Mungu juu ya Mwanae. 11 Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uzima wa milele, na uzima huo uko kwa Bwana. 12 Yeyote, aliye na Mwana wa Mungu anao uzima huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana uzima. 13 Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uzima wa milele ninyi mnaoamini kwa jina la Mwana wa Mungu. 14 Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya mapenzi yake, yeye hutusikiliza. 15 Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba atupatia yote tunayomwomba. 16 Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo anapaswa kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uzima. Nasema jambo hili kuhusu wale waliotenda dhambi ambazo si za kifo. Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu kwenye kifo nami sisemi kwamba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo. 17 Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu kwenye kifo. 18 Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. 19 Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule Mwovu. 20 Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli—katika muungano na Mwanae, Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uzima wa milele. 21 Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu.
<- 1 YOHANA 4